Mapinduzi Cup: Sure Boy arejea kikosini kuwaangamiza URA

Kiungo mchezeshaji wa timu ya soka ya Azam Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amejiunga na kikosi katika mazoezi maalumu kujiandaa na mchezo wa fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup utakaopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Sure Boy amerejea kikosini baada ya kukosa michezo kadhaa kutokana na kupatwa na msiba wa mama yake mzazi Januari 3 mwaka huu, na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kuumana na URA ya Uganda.

-Mchezaji Salumu Abubakar ambaye alikwenda Dar es Salaam kwa ajili ya msiba wa mama yake amerejea na tayari amejiunga na kikosi, na ameshiriki vyema katika mazoezi ya mwisho tuliyofanya Ijumaa, amesema afisa habari wa Azam Jaffary Idd Maganga.

Katika hatua nyingine Azam imewaomba watanzania wote bila kujali tofauti zao katika upenzi wa soka kuwaunga mkono ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kubakisha kombe hilo nyumbani.

Afisa habari wa Azam Jaffary Maganga amesema watanzania wote wanapaswa kuona kuwa sasa vita imekuwa ni ya Tanzania na Uganda katika mchezo huo hivyo ni muhimu kuiunga mkono timu yao ya nyumbani na kusahau yaliyopita.

-Ni muda muafaka kwa Watanzania kuiombea dua timu ya Azam lakini vile vile kuwapa morali wachezaji wetu, katika muonekano na sura ya mashindano hivi sasa ni kama vita ya nchi mbili Tanzania na Uganda hivyo tunahitaji sana support yao, amesema.

Taji la nne.

Mchezo huo wa fainali utafanyika kuanzia majira ya saa 2:15 usiku ambapo kama Azam wataibuka na ushindi basi watakuwa wamejiwekea historia ya kwao wenyewe ya kutetea taji hilo kwani waliwahi kufanya hivyo mwaka 2012 na 2013.

Mwaka 2012 Azam waliingia fainali na kuifunga Jamhuri Pemba kwa mabao 3-1 wakati mwaka 2013 walichukua taji kwa kuichapa Tusker FC ya Kenya mabao 2-1.

Kwa Upande wa URA kama watafanikiwa kutwaa taji, litakuwa ni taji la pili baada ya lile walilolitwaa mwaka 2016 kwa kuwafunga wakata miwa wa Turiani mkoani Morogoro Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.

Related news
related/article
Local News
Lwandamina adaiwa kuikacha Yanga na kurejea Zesco United
10 Apr, 17:35
Local News
VPL: Raundi ya 24, mtoto hatumwi sokoni
10 Apr, 16:55
Local News
AFCON U20 Q: Kabwili kujiunga na wenzake Jumatano
10 Apr, 07:40
Local News
VPL: Lipuli waifuata Mwadui, Mnyate akiugua
09 Apr, 09:45
Local News
Breaking News: Rufaa ya Wambura yagonga mwamba
06 Apr, 12:55